HABARI ya kufungia mwaka 2013 na kufungua pazia la mwaka mpya wa 2014
ni madai ya mwanamitindo kiwango Bongo, Jacqueline Patrick kukamatwa
katika Uwanja wa Ndege wa Macau nchini China akiwa na mzigo wa madawa
ya kulevya aina ya heroin lakini Risasi Mchanganyiko linaangaza mapya
zaidi juu ya sakata hilo.
Mwanamitindo Jacqueline Patrick.
Macho na masikio ya Wabongo wengi kwa sasa ni juu ya mwenendo wa
madai hayo, wakati gazeti hili likiendelea kupekenyua limenasa mpya
kuwa, Jack yupo kwenye mateso makali kutoka kwa askari wapelelezi nchini
humo wanaotaka kujua mtandao unaomuunganisha katika mchezo huo.
SAUTI KUTOKA CHINA
Chanzo chetu makini kilichopo China ambacho
kinapiga kitabu kilieleza kuwa, katika kufuatilia ishu hiyo, juzi
Jumatatu, Desemba 30, 2013, alikutana na kizingiti cha kushindwa kuonana
na Jack katika mahabusu aliyowekwa kwa maelezo kwamba, uchunguzi bado
unaendelea.
Dawa za kulevya zilizokutwa tumboni mwa Jack.
Raia huyo wa Tanzania aliyedai ana ukaribu na Jack, kwa sharti la
kutochorwa jina lake gazetini, alisema mengi kuhusiana na mateso
anayopata mrembo huyo hivi sasa.
“Ni kweli Jack amekamatwa hapa
Macau. Hilo halina ubishi kabisa. Sheria za huku zinatofautiana kati ya
jimbo na jimbo. Nilifika mahabusu aliko kwa lengo la kutaka kumwona
lakini nilikataliwa. Nimeambiwa hawezi kuonana na mtu yeyote hadi Machi,
mwakani (mwaka huu). Bado wanaendelea na uchunguzi kwanza.
“Unajua wanajaribu kufichaficha mambo ili polisi waweze kufanya
upelelezi wao vizuri lakini nimepenyezewa taarifa kuwa ataingizwa chumba
cha mateso ili abanwe na kutaja mtandao wake. Wanajua yeye
wameshamkamata, lakini wanataka kufahamu mzigo alitumwa na nani, ameutoa
nchi gani na unakwenda nchi gani?
“Lengo la kufanya hivyo ni kukomesha mtandao mzima wa madawa ya
kulevya. Si ajabu akawa kwenye mateso kwa kipindi chote hicho kama
hatakuwa mkweli lakini kwa sasa ataingizwa kwenye kikosi cha kwanza.
Jack akiwa chini ya ulinzi.
“Hapo atakalishwa kwenye chumba cha mateso kwa siku mbili mfululizo
(akimaanisha saa 48). Ni mateso makali sana. Wataalam wanajua
wanafanyaje ili mtuhumiwa aweze kuzungumza ukweli kwa muda mfupi. Sasa
hapo ikishindikana ndipo anaweza kuhamishiwa kwenye kikosi kingine,”
alipasha mtoa habari wetu na kuongeza:
“Ni kama huko Bongo tu. Unaposikia chumba cha mateso ya wapelelezi
maana yake shughuli yake siyo ndogo. Mimi namuonea huruma sana Jack,
lakini najiuliza, hivi ni kwa nini huwa hawajifunzi kupitia wenzao?
“Si juzi tu wengine (Agnes Gerald ‘Masogange’ na Melisa Edward)
wamekamatwa kwa madawa hayohayo na walisota kwa muda mrefu? Kwa nini
hawasikii jamani? Namuhurumia sana kwakweli.”
KUMBE DADA YAKE ALIMUONYA
Habari
kutoka kwa mtu wa karibu na dada wa Jack zinasema kuwa, wakati akitaka
kusafiri akitokea Bongo, alimweleza dada yake juu ya mpango wake huo,
akamuonya lakini modo huyo alikataa.
“Alimfuata dada yake na kumweleza mchongo mzima kuwa alitaka kwenda
na mzigo China, dada yake akamwambia aachane na hizo biashara, akakataa.
Jack alifikia hatua akamwambia dada yake kuwa hana mtoto, hana mume
wala ndugu anayemtegea kwa hiyo yupo tayari kwa lolote kwani hakuwa na
cha kupoteza.
“Kama angemsikiliza dada yake (jina linahifadhiwa) haya yote
yasingemkuta na asingeingia kwenye mateso ya namna hii,” alisema mtoa
habari wetu huku akiendelea kusisitiza jina lake lisionekane mahali
popote kwenye ukurasa huu.
ABEBESHWA MZIGO, ALIPWA MALIPO YA AWALI
Ilizidi kusemekana kuwa,
alipokaribia kuondoka Bongo, Jack alimwambia dada yake kwamba anakwenda
kambini (kituo cha kuingiza mzigo tumboni) ambapo aliporejea kwa
dada’ake alimuonesha dola za Kimarekani 21,000 (zaidi ya shilingi
milioni 33) ambazo ni malipo ya awali huku akimwambia alishabebeshwa
nusu ya mzigo.
Hata hivyo, habari zinasema Jack alimwambia dada yake huyo kuwa
hakuwa akijisikia kusafiri lakini kwa kuwa anatafuta maisha aliamua
kuondoka baada ya mzigo kukamilika wote siku iliyofuata.
INA MAANISHA NINI?
Kwa mujibu wa maelezo hayo, Jack aliondoka na
unga hapahapa Bongo kwenda Thailand kupitia Nairobi, Kenya na baadaye
Macau, China ambako alinaswa.
MASTAA WAFUNGUKA
Watu wamekuwa na mitazamo tofauti kulingana na
ishu hiyo lakini Risasi Mchanganyiko lilipata nafasi ya kuzungumza na
baadhi ya mastaa wa Bongo ambao wameeleza maoni yao kuhusiana na sakata
hilo la Jack.
Katika mahojiano na waandishi wetu, tulitaka kusikia kutoka kwao
namna wanavyolinganisha tabia ya kujihusisha na biashara za kusafirisha
madawa ya kulevya na vitendo vya umalaya ambapo wametoa maoni tofauti.
JACQUELINE WOLPER:
“Mh!
Mwenzangu, bora uwe na mabuzi (wanaume wenye mkwanja) 40 kuliko kufanya
biashara ya madawa ya kulevya. Nawaomba mastaa wenzangu wasikubali
kubebeshwa madawa kwa kudanganywa eti na dola 30,000, kamwe haiwezi
kubadili mfumo wa maisha yako.”
REHEMA CHALAMILA ‘RAY C’:
“Madawa
ya kulevya hayakubaliki, yalinitenda sana haya madude! Kabisa tulinde
vizazi vijavyo kwa kupiga vita madawa ya kulevya. Fanya yote lakini siyo
madawa ya kulevya.”
SHAMSA FORD:
“Nasema hivi, bora umalaya
japo pia si mzuri kuliko kudili na biashara ya madawa ya kulevya.
Nawaomba waachane na vitu hivyo kwani vinatumaliza kisanii... lakini
nasisitiza kutulia na bwana mmoja ni vizuri sana kuliko kurukaruka.”
JOKATE MWEGELO:
“Hakuna
aliye mkamilifu lakini kama kitu ni kiovu ni kiovu tu hata kama mimi na
wewe tunakifanya, kimsingi hakuna bora na anayesema kuna ubora basi
hajitambui. Vyote vinadhalilisha utu na thamani ya mwanamke. Mwili si wa
kuchezewa.”
BLANDINA CHAGULA ‘JOHARI’:
“Tukitumia majina yetu
vizuri, hakuna atakayejihusisha na yote hayo... tujitume kufanya kazi,
umalaya unaweza kuwa bora kuliko kufanya biashara ya madawa ya kulevya
kama utabanwa kuchagua maovu hayo. Maisha ya Ughaibuni yatatumaliza
kwani tunaiga kwa kukurupuka bila kuelewa.”
TUMETOKEA HAPA
Jack
anatuhumiwa kukamatwa na madawa ya kulevya Desemba 19, 2013 katika
Uwanja wa Ndege wa Macau, China akitokea jijini Bangkok, Thailand akiwa
safarini kwenda Guangzhou nchini China.
Ilielezwa kuwa unga aliokutwa
nao una uzito wa kilo 1.1 ndani ya kete 57 huku thamani yake ikitajwa
kuwa ni zaidi ya shilingi milioni 223.
Bado yupo mikononi mwa polisi
wa China wakati upelelezi wa awali ukiendelea ambao utafikia tamati
Machi, mwaka huu kabla ya kuingia hatua inayofuata.
-Risasi