Tuesday, 29 October 2013

MWIGAMBA ALIA NA UBAGUZI NDANI YA CHADEMA, ASHAURI MBOWE AJIUZULU...

Samson Mwigamba.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Arusha, Samson Mwigamba, ambaye amesimamishwa kwa muda usiojulikana, ameelezea namna uongozi wa juu wa chama hicho, unavyobagua watu wa kuwaadhibu wakati wa kutoa maoni kuhusu chama.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Mwigamba pia alikiri kutoa maoni katika mtandao wa Jamii Forum, huku akificha jina lake, akiwasiliana na wanachama wenzake.
Alisema kwa sasa ni vema uongozi uliopo upumzike na kuwaachia wengine, kama walivyofanya viongozi wote waliotangulia.
Alisisitiza kwamba alimaanisha alichokiandika na alikuwa habahatishi.
Alitaka wanachama wenzake, waelewe kuwa ni kawaida kiongozi akiwa na maoni yanayohusu mambo ya ndani anayotaka wanachama wenzake wayapate bila kuhusisha cheo chake, huchagua njia yoyote ambayo ataona inafaa, ikiwa ni pamoja mitandao ya jamii kwa kuficha jina lake.
Kawaida hiyo kwa mujibu wa Mwigamba, imetokana na Katiba ya Chadema, kukataza viongozi kutoka hadharani na kuzungumza mambo ya chama, badala yake watumie vikao.
Hata hivyo, kwa mujibu wa kiongozi huyo ambaye amewahi kufanya kazi makao makuu ya Chadema, vikao hivyo vimeshindwa kushughulikia udhaifu wa uongozi kwa kuwa kila anayejaribu kuhoji, hutangazwa kuwa msaliti wa chama.
“Ni wajumbe wachache sana kwenye Kamati Kuu kwa mfano ambao bado wanaweza kusimama kidete na kukosoa uongozi, watu hao hawazidi watatu au wanne, ambao ni Dk Kitila Mkumbo, Profesa Mwesiga Baregu, Mzee Shilungushela (amemtaja kwa jina moja) na mzee Sgerembi ambaye sasa ni marehemu,” alisema Mwigamba.
Alisisitiza kuwa viongozi wengi ndani ya Chadema, wanayo majina yasiyojulikana kwenye mitandao ya jamii na huyatumia  kuzungumza na wanachama mambo mengi, ambayo hawataki yahusishwe na vyeo vyao na mambo hayo hubaki kuwa maoni ya mwanachama binafsi.
Alisema kama angetoka kwenye vyombo vya habari na kujitambulisha na kuanza kuzungumza yale aliyoandika, viongozi wangekuwa na haki ya kumshitaki kwenye mamlaka yake ya nidhamu.
Lakini, alidai hakuna mtu yeyote awe mtaalamu wa Teknolojia ya Habari, au vyovyote vile, mwenye haki ya kwenda  kwenye  mtandao  na kuanza kutafuta anuani kufahamu kilichoandikwa kimetoka kwenye kompyuta gani au nani katuma.
Aliutaka uongozi huo, ueleze wanaofanya kazi ya kufuatilia kila mtu anayetoa maoni kuhusu chama katika mtandao, wametumwa na nani?
“Je wanachunguza na kuingilia mawasiliano ya watu wameajiriwa na nani na kazi hiyo wameianza lini na wameshapata watu wangapi?” Alihoji.
Alisema hata kama wameanza kazi hiyo Ijumaa iliyopita na mtu wa kwanza kumpata akawa yeye, wamueleze baada tu ya tukio hilo, wameshapata wengine wangapi, maana bado viongozi wengine wanaendelea kufanya kama alivyofanya yeye.
“Au kuna mtu ama watu fulani ndani ya chama, ukiwagusa tu ndio unatafutwa au kuitwa msaliti wa chama?” Alihoji.
Alisema miezi kadhaa iliyopita, kuna viongozi walijitokeza katika mitandao na kueleza kwa kurudia rudia udhaifu wa viongozi wa chama, akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto lakini hivi sasa mmojawapo kati ya watu waliosemwa sana kupitia mtandao huo (hakumtaja jina), amepandishwa cheo na kuwa Ofisa wa Makao Makuu ya chama hicho.
"Siku zijazo tutakuwa na madikteta ambao watatumia demokrasia kujihalalishia utawala wa milele ndani ya vyama vyao na hata ndani ya nchi na ikiwezekana kurithishana utawala kutoka kwa baba kwenda kwa mtoto, mtoto kwenda mkwe kama ilivyo sasa,” alisema huku akisisitiza kuwa alichoweka katika mtandao alimaanisha
Katika mtandao Mwigamba alimpongeza Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe kwa kufanya mengi katika chama hicho.
Alitaja baadhi kuwa ni pamoja na kutoa chama kutoka kuwa cha tatu ama nne kwa upinzani hadi kuwa cha kwanza na kustahili kuitwa chama kikuu cha upinzani.
“Kakichukua kikiwa na wabunge watano bungeni na leo katika kipindi chake cha miaka 10, kina wabunge 49. Ni mafanikio makubwa! Si hivyo tu, ni wakati wake Chadema imebeba ajenda nzito za kitaifa kama vile vita dhidi ya ufisadi, utetezi wa rasilimali, Katiba mpya na kadhalika,” alisema.
Hata hivyo, alisema  kuna matatizo yameanza kujitokeza na wanachama wasipochukua hatua haraka, huko mbele watapata shida kubwa. Alimtaka  Mbowe kuelewa kwamba uwezo wake umefikia hapo, asitake kulazimisha kusonga mbele, akidhani bila yeye hakuna Chadema.
“Akiache chama kikiwa salama, abaki kama Mwenyekiti mstaafu na awaachie wengine awamu inayofuata ya kuingia madarakani. Kama hataki kuwa mwelewa na kuachia ngazi, wanachama tumsaidie kwa kumpiga chini uchaguzi ujao,” sehemu ya andiko hilo la Mwigamba ilieleza.

0 comments:

Post a Comment