WAKATI
Serikali ya Marekani ikiwa bado inapona majeraha ya mgogoro wa
kidiplomasia na nchi washirika wake wa karibu barani Ulaya kutokana
madai ya kufuatilia mawasiliano ya viongozi wa mataifa hayo, Ikulu ya
Jijini Dar es Salaam imesema haijui kama mawasiliano ya Rais Jakaya
Kikwete pamoja na viongozi wengine hapa nchini yanafuatiliwa na
Marekani.
Tamko hilo la Ikulu limekuja wakati
tayari hali ya mashaka imetawala kwa viongozi pamoja na watu wa kada
mbalimbali hapa nchini, kwamba ushirika wa karibu uliopo kati ya
Tanzania na Marekani unaweza kuwa ni kigezo cha taifa la Marekani
kufanya udukuzi wa mawasiliano yao.
Ni kutokana na hali hiyo, RAI Jumapili
lilimtafuta Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, ambaye
alisema: “Ikulu haijui lolote kama mawasiliano ya Rais Kikwete
yanafuatiliwa, labda waulizeni wao...kwa ushauri tu nawaombeni muandike
mambo ya msingi, kwa hiki mnachokifanya sidhani kama ni sahihi”.
Gazeti hili, wiki iliyopita liliripoti
juu ya kuwepo kwa hali hiyo ya shaka, kutokana na urafiki wa muda mrefu
uliopo kati ya Tanzania na Marekani, ambapo kwa nyakati tofauti, marais
watatu wa taifa hilo kubwa duniani wamepata kuzuru nchini.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania, Profesa John Nkoma, alipotafutwa na gazeti hili kuhusiana na
taarifa hizo, si yeye wala wasaidizi wake walioweza kupatikana mara
moja, licha ya gazeti hili kutumia mbinu mbalimbali kuwafikia.
Kwa takribani wiki tatu sasa, Marekani
imejikuta katika mzozo mkubwa wa kidiplomasia na baadhi ya mataifa ya
Ulaya, baada ya kuibuka madai kuwa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel,
simu zake zimekuwa zikifuatiliwa kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.
Kauli tofauti ambazo zimepata kutolewa
ndani ya wiki iliyopita na majasusi wa mataifa makubwa duniani, ikiwemo
Marekani na Uingereza, wakati wakizungumzia madai ya Marekani kufuatilia
mawasiliano ya Kansela Merkel, kwamba nchi zote duniani zinachunguzana,
ndiyo ambayo ilijenga shaka kwamba Tanzania huenda ikawa kwenye orodha
hiyo ya kufuatiliwa.
Kwa mujibu wa majasusi hao,
waliozungumza na Shirika la Habari la NBC kwa sharti la kutotajwa majina
yao, nchi zote duniani zinachunguzana na kwamba kinachodaiwa kufanywa
na Marekani si cha kushangaza.
Kauli hiyo ndiyo ambayo baadhi ya
wafuatiliaji wa mambo wanadai kuwa Tanzania bila shaka haiwezi kukwepa
kufuatiliwa na majasusi wa Marekani, ambao hufanya hivyo kwa nia ya
kujiridhisha usalama na urafiki uliopo baina yao.
Mbali na hilo, kauli iliyowahi kutolewa
na mfanyakazi wa zamani wa shirika la kijasusi la Marekani la NSA,
Edward Snowden, kwamba ujasusi huo wa Marekani haufanywi dhidi ya
watuhumiwa wa ujasusi na wakazi wa nchi zenye ugomvi na Marekani tu,
bali hata marafiki na waitifaki wa karibu kabisa na nchi hiyo, ndiyo
ambayo inajenga mazingira ya Tanzania nayo kuwemo kwenye orodha hiyo ya
kufuatiliwa.
Marais watatu wa Marekani kwa nyakati tofauti wamepata kuzuru nchini, wawili kati yao ni kabla na baada ya kuondoka madarakani.
Marais hao ni Bill Clinton, George W. Bush na Barack Obama.
Bill Clinton, aliyezuru nchini mwaka
2000, wakati huo akiwa Rais, George W. Bush mwaka 2008, wote kwa pamoja
kwa nyakati tofauti na kwa zaidi ya mara moja wamepata kutembelea nchini
kabla na baada ya kuondoka madarakani.
Kwa upande wake, Rais wa sasa, Barack Obama, alitembelea nchini Julai mwaka huu na kuiacha Kenya, nchi ambayo ni asili yake.
Ni kutokana na hilo, hulka ya vyombo
vya usalama vya Marekani kutaka kujiridhisha usalama kwa viongozi wao
haiwezi kuwatenga na suala zima la kufanya udukuzi wa mawasiliano katika
nchi ambazo viongozi wake wanatembelea au kutembeleana.
Kwa muktadha huo, tayari baadhi ya
wachambuzi waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina
yao gazetini, wanasema kuwa uwezekano wa Marekani kufuatilia mawasiliano
ya viongozi wa hapa nchini, akiwemo Rais wa sasa, Jakaya Kikwete ni
mkubwa na ni jambo lisilo la kushangaza.
Wachambuzi hao wanazilinganisha taarifa
za sasa za udukuzi wa mawasiliano unaodaiwa kufanywa na Marekani na
mchezo ambao ulipata kufanywa huko nyuma na mtandao wa Weakleaks dhidi
ya Tanzania.
Mtandao huo umepata kuwagusa viongozi
wa serikali, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, ukitoa taarifa za siri
ilizodai kuzinukuu kutoka kwa baadhi ya maofisa wa Ubalozi wa Marekani
nchini.
Juni mwaka huu, mwanausalama aliyeasi
wa Marekani, Edward Snowden, alitoboa siri ya idara za usalama nchini
humo kwamba zimekuwa zikifuatilia mawasiliano ya simu na barua pepe kwa
watu mbalimbali duniani kote, wakiwamo viongozi wenye ushirika wa karibu
na taifa hilo.
Hata hivyo, Marekani imekana kufanya
udukuzi kwa namna ambayo imetafsiriwa na baadhi ya washirika wake na
badala yake imedai kuwa udukuzi ambao imekuwa ikiufanya ni wa kawaida
kwa ajili ya usalama na kwamba wamekuwa wakirejesha taarifa zote kwa
nchi husika.
Mkurugenzi wa Idara ya Usalama ya
Marekani, James Clapper, wiki iliyopita alikaririwa akisema upelelezi wa
Marekani katika mataifa ya kigeni huwa haufanywi kiholela.
-Mtanzania
0 comments:
Post a Comment