UTARATIBU wa Chadema kutumia kinachoitwa ‘nguvu ya umma na vurugu’ kushinikiza sheria ipindishwe kwa maslahi yake, umekwama kumnusuru Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli anayetumikia adhabu ya kukaa jela kwa siku 14.
Jana
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Sylvester Masinde, alikiri
kuwa nguvu ya umma iliyodaiwa kutumika kumnusuru Machemli, ni upotoshaji
na hali ilivyokuwa, mamlaka zilishajiandaa kukabiliana nao.
Kutokana
na hali halisi, Masinde alisema chama hicho hakiwezi na wala hakina
mpango wa kutumia nguvu ya umma, kushinikiza Machemli atoke mahabusu.
Masinde
alifikia hatua ya kuwambia viongozi wa ngazi ya msingi wa chama hicho
kuwa ni vema utaratibu uliowekwa kisheria uheshimiwe.
Kiongozi
huyo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, alisema suala
hilo limechunguzwa na kubaini ni kweli Machemli aliruka dhamana, hivyo
Mahakama Kuu pekee ndiyo yenye mamlaka ya kutengua uamuzi huo.
Machemli
anakabiliwa na kesi ya uchochezi na Novemba 6 aliamriwa na Mahakama ya
Wilaya kwenda rumande kwa siku 14, baada ya kuidharau kwa kutotokea
wakati kesi ikiitwa.
Tofauti
na ilivyokuwa kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ambaye alisema
lupango ndiko kwenye wapiga kura wake, kwa Machemli Chadema imeamua
kufuata utaratibu kumtoa.
Kabla
ya kuahirisha kesi hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Faustine Kishenyi aliagiza mbunge huyo baada ya siku 14 afikishwe tena
mahakamani hapo akiwa na wadhamini wengine watatu ambao kila mmoja
atatakiwa kuwa na hati ya nyumba.
Mamlaka
zajiandaa Katika hatua nyingine, kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa
Chadema alikiri kuwa mamlaka wilayani humo, zilishajiandaa kukabiliana
na nguvu ya umma.
Alidai
alifuatana na viongozi wengine wa chama hicho kwenda kumjulia hali
mbunge huyo, lakini barabarani walikuwa wakifuatwa kwa karibu na gari la
Polisi. Hata hivyo, walipofika gerezani, walitakiwa na Mkuu wa Gereza
waondoke.
Akizungumzia
sababu za kuzuiwa kuingia gerezani hapo, kiongozi huyo alidai anahisi
pengine mamlaka husika zilitishwa na uvumi usio wa kweli kuwa
zingetumika nguvu za umma kushinikiza Mahakama itoe dhamana kwa mbunge
huyo.
Hata
hivyo, Mkuu wa Magereza wa Wilaya, Edward Nyabange, alisema viongozi
hao wa Chadema wakiwa zaidi ya 10 walizuiwa kuingia gerezani hapo kwa
sababu ya kutofuata utaratibu.
Alisema
utaratibu uliopo unaelekeza Jumapili pekee ndiyo mahabusu na wafungwa
wanaruhusiwa kutembelewa na jamaa zao na kuongeza kuwa mbali na viongozi
hao kuvunja utaratibu, pia idadi yao ilikuwa kubwa.
-Habari leo
-Habari leo